Baada ya Serikali kumwekea pingamizi mahakamani Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe katika maombi yake ili asikamatwe na hatimaye yakatupwa,
imemwekea kigingi kingine kwenye kesi ya msingi.
Mbowe amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mkuu wa
Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG).
Katika kesi ya msingi namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe pamoja na mambo
mengine anapinga mamlaka ya mkuu wa mkoa kukamata na kile anachokiita
kudhalilisha watu.
Hivyo, anaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine itamke kuwa
vifungu namba 5 na 7 vya Sheria ya Tawala za Mikoa vinavyowapa mamlaka
wakuu wa mikoa na wilaya kuwakamata watu na kuwatia mbaroni viko kinyume
cha Katiba.
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu
likiongozwa na Sekieti Kihiyo akisaidiana na Pellagia Kaday na Lugano
Mwandambo, ilitajwa jana na upande wa Serikali ukawasilisha pingamizi la
awali, ukiiomba mahakama iitupilie mbali.
Kutokana na pingamizi hilo, pande zote walikubaliana kusikiliza
pingamizi hilo kwa njia ya maandishi, mahakama ikaamuru upande wa
Serikali uwasilishe mahakamani hapo hoja za pingamizi Machi 17.
No comments:
Post a Comment