Rais
wa Malawi, Peter Mutharika ameanza tena chokochoko baada ya kutangaza
kuwa hakuna nchi ambayo inamiliki kwa pamoja Ziwa Nyasa na kwamba
haijafikia makubaliano na nchi yoyote, hivyo ameahidi kulinda umiliki na
masilahi yake.
Kauli
hiyo ni tofauti na mazungumzo ya Mutharika na Rais John Magufuli
yaliyofanyika Januari 30 jijini Addis Ababa, Ethiopia wakati walipokuwa
wakihudhuria kikao cha Umoja wa Afrika (AU).
Katika
taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Rais baada ya kikao
hicho, ilisema marais wote wameridhishwa na jitihada zinazofanywa na
jopo la usuluhishi lililoteuliwa na Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini
mwa Afrika (Sadc).
Jopo hilo linaongozwa na rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mindi Kasiga amekiri kuiona taarifa hiyo na alisema anayeweza kulizungumzia suala hilo ni Naibu Waziri.
“Tumeiona
hiyo taarifa ila jaribu kumtafuta Naibu Waziri maana Waziri atakuwa nje
ya nchi. Ninachofahamu baraza la usuluhishi bado linaendelea na vikao
vyake. Ukimpata naibu waziri atakuwa na maelezo ya kina.”alisema Mindi.
Lakini,
akihudhuria Siku ya Maji Duniani Jumatano iliyopita mjini Mangoshi,
Rais Mutharika alisisitiza msimamo wa Malawi kulinda umiliki wa ziwa
hilo dhidi ya watu aliowaita wavamizi.
Mutharika
alisema Malawi ndiye mmiliki pekee wa Ziwa Malawi, ambalo huku
linajulikana kama Ziwa Nyasa, na kuonya kuwa utawala wake hautavumilia
watu watakaokuwa na nia ya kuyumbisha taarifa za umiliki.
“Hebu
tulilinde ziwa letu. Hili ni ziwa letu na ninaposema ziwa letu
namaanisha ziwa lote. Mtu yeyote asifanye kosa la kubadili umiliki ambao
umekuwepo kwa miaka 124 iliyopita,” alisema Mutharika akikaririwa
na tovuti ya Nyasa Times ya Malawi juzi wakati wa mkutano huo
uliofanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Nkopola Lakeshore mjini
Mangochi.
“Tunathamini ziwa letu na tutahakikisha tunachukua hatua za kulilinda kwa gharama zozote,” alisema.
Mutharika
aliwataka wananchi kupunguza matumizi mabaya ya maji ili yapatikane kwa
ajili ya kilimo na viwandani wakati wa msimu wa ukame.
Hivi
karibuni, Malawi na Tanzania zimejikuta katika mzozo wa umiliki wa Ziwa
Nyasa lililo kusini mwa Tanzania, mzozo ambao umesababisha kuanza kwa
mazungumzo ya usuluhishi kumaliza kutokubaliana huko baada ya nchi hizo
mbili kushindwa kufikia muafaka. Mzozo wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa
umekuwepo tangu mwaka 1967.
Lakini, mzozo wa hivi karibuni umeibuka baada ya Malawi kuanza utafiti wa mafuta na gesi kwenye ziwa hilo.
Hata
hivyo, Mutharika alisema uchimbaji mafuta utaendelea katika ziwa hilo
licha ya wanaharakati wa mazingira kuitaka Malawi iache mpango huo.
“Wale
wanaohofia kuhusu mipango yetu ya kutafuta na kuchimba mafuta hawana
sababu ya kuhofia. Kama tutaamua kuchimba mafuta katika ziwa,
tutahakikisha tunatumia teknolojia safi,” alisema akikaririwa na Nyasa Times.
No comments:
Post a Comment