Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa waraka uliojumuisha mambo mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi kutenda haki, kutokuwa na
upendeleo, kuheshimu Katiba na sheria za nchi.
Pia
jumuiya hiyo imewataka Watanzania kwa ujumla kuliombea taifa na
viongozi wake, ili wawe walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama
walivyoapa.
Waraka
huo ulisambazwa jana katika vyombo vya habari, ukiwa umetiwa saini na
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk.
Fredrick Shoo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania (KAT), Dk.
Jacob Chimeledya.
Wengine
ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Dk. Isaac Nicodemo
na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church in Tanzania (AICT),
Silas Kezakubi.
“CCT
inatoa maelekezo kwa Wakristo wa makanisa wanachama na Watanzania wote
kwa ujumla, kuendelea kulinda na kuheshimu misingi ya haki za binadamu
na kuliombea taifa na viongozi wake ili waendelee kuwa na hofu ya Mungu
na waadilifu.
“Watende haki, wasiwe na upendeleo na waheshimu na kuwa walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa,” ilisema sehemu ya waraka huo.
CCT
ilieleza pia kusikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha
katika jamii na kukemea matukio ya ukatili na yale ya watu kupotea
katika mazingira ya kutatanisha.
“CCT inasikitishwa na vitendo vya ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii yaliyofikia kiwango cha kuua askari polisi."
Aidha, CCT inakemea matukio ya ukatili unaondelea katika jamii.
“Yapo
matukio ambayo yamedhihirisha ushirikiano hafifu kati ya polisi na
wananchi na kuendelea kujitokeza kwa matukio yanayoashiria chuki za
kidini na kikabila.
“CCT
inatoa wito kwa Serikali kuhakikisha misingi ya umoja na mshikamano wa
kitaifa inaheshimika na utawala wa kisheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.
CCT
ilisema ili vita dhidi ya dawa za kulevya ifanikiwe, ni muhimu Serikali
ikalenga kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata wahusika wakuu wa
biashara hiyo bila kujali wasifu wao na nafasi walizonazo katika jamii.
Kutokana
na hilo, CCT ilisisitiza kuwa Serikali izingatie misingi ya sheria,
haki na usawa katika kuwakamata, kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo
vya sheria bila kuonea mtu wala kusukumwa na misingi yoyote ya imani au
itikadi ya mtu.
“CCT
inaunga mkono vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na viroba
iliyoanzishwa na Serikali. Hata hivyo, CCT inasisitiza kuwa ili vita hii
ifanikiwe, ni muhimu sana Serikali ilenge kutokomeza kiini cha tatizo
kwa kuwapata wahusika wakuu wa biashara hii bila kujali wasifu wao,
nafasi zao wala nafasi walizo nazo katika jamii.
“Katika
kufanya hivyo, ni muhimu Serikali izingatie misingi ya sheria, haki na
usawa katika kuwakamata, kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria bila kuonea wala kusukumwa na misingi yoyote ya imani au itikadi
ya mtu.
“Ni
muhimu kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana
kupata ajira na kuendesha shughuli za ujasiriamali ili kujiepusha na
vitendo viovu vikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na unywaji wa pombe
kali.
“CCT
inayaelekeza makanisa wanachama, wazazi na walezi kuendelea kuwalea
vijana wao katika misingi ya kidini ili wasijiingize katika matumizi ya
dawa za kulevya na pombe kali.
“Wakati
huu wa Kwaresma, tunawaombea na kuwaomba wale wote ambao kwa njia moja
au nyingine wanajihusisha na dawa za kulevya au unywaji wa pombe kali,
watubu na kuyaacha maovu yao na Mungu atawarehemu,” walisema maaskofu hao.
Hali ya Chakula
Kuhusu
hali ya chakula nchini, CCT ilisema kuwa pamoja na mvua kuanza
kunyesha, Serikali na wengine wawezeshe usambazaji wa chakula kutoka
mikoa yenye ziada kwenda mikoa yenye uhaba wa chakula ili bei ya chakula
iweze kushuka.
“Tunaiomba
Serikali kupitia idara yake inayohusika, iratibu na kusaidia
utekelezaji wa jambo hili, ili wananchi waweze kumudu bei, mfano mahindi
hayo yakisambazwa, bei ishuke kutoka zaidi ya Sh 100,000 ifikie angalau
Sh 60,000.
“Pia
tunawaomba wakulima wasitumie njaa hii kutekeleza usemi ya kwamba ‘kufa
kufaana’, hivyo kwao kipindi hiki kigumu kwa Watanzania wengine
wakakifanya kipindi cha kupandisha bei ili kupata faida kubwa.
“Sambamba
na wito huu, tunawaekeleza wanachama wetu kupitia vitengo vya maafa na
misaada ya kibinadamu, waendelee kuwasaidia wananchi wenye upungufu
mkubwa wa chakula wakipate kwa bei nafuu kwenye maeneo yao,” ilisema.
CCT iliwataka Wakristo wote kuendelea kumwomba Mungu ili mvua zinazoendelea kunyesha ziwe za neema na zisilete madhara.
Katika
hilo, wameiomba serikali kutoa unafuu wa bei ya gesi ya kupikia ili
wananchi wengi wapunguze au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa.
Elimu
CCT
ilisema pamoja na nia njema ya Serikali kutoa elimu bure, lakini
iangalie masilahi ya walimu na kuwe na mpango mkakati unaotekelezeka wa
kuimarisha miundombinu ya kufundishia.
“Serikali
haina budi kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu dhana
ya elimu bila malipo, ili kuepusha migogoro inayokabili sekta ya elimu
kwa dhana hiyo kutoeleweka kwa vizuri kwa baadhi ya wananchi.
“Pia
mabadiliko ya mitaala na miongozo mingine ya kufundishia ya mara kwa
mara imekuwa ikiathiri elimu ya Tanzania kwa kila awamu ya uongozi na
kuwafanya wahitimu wetu kukosa ushindani kikanda na kimataifa,” ulisema waraka huo.
Kupitia
waraka huo, maaskofu waliishauri Serikali kuwa na será ya elimu
isiyobadilika badilika kila uongozi mpya unapoingia madarakani.
No comments:
Post a Comment