Monday, March 13, 2017

KINANA ATWISHWA ZIGO


                                                ABDULRAHMAN KINANA.

HUSSEIN Bashe, Joseph Musukuma na Adam Malima wamekataa kuzingumzia kushikiliwa na kuhojiwa kwao na Jeshi la Polisi na kusema suala hilo wamemwachia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Bashe na Musukuma ni wabunge na Malima aliyewahi kuwa mbunge pia katika awamu iliyopita, juzi walitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma wakituhumiwa kupanga njama mbaya dhidi ya chama hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, aliiambia Nipashe juzi kuwa walilazimika kuwakamata na kuwatia mbaroni watatu hao kufuatia taarifa kuwa walikuwa wanafanya njama za uchochezi ili pawe na vurugu wakati wa mkutano mkuu maalumu wa CCM uliofanyika jana mjini Dodoma.

Hata hivyo, wakizungumza na Nipashe kwa simu kwa nyakati tofauti wakiwa mjini Dodoma jana, makada hao wa CCM walisema hawawezi kueleza kilichowafanya wakamatwe, kuhojiwa na baadaye kuachiwa na polisi kwa kuwa maelezo yote yako kwa Kinana.

Mbunge wa Nzega Mjini, Bashe alisema: "Kilichotokea ni mpango wa Mungu. Suala hili ataongea Katibu Mkuu wa CCM (Kinana).

Mtafuteni Kinana, maana yeye ndiye anajua kama kuna hatua zozote za kichama zitazochukuliwa dhidi yetu."

Mbunge wa Geita, Musukuma alisema: "Mpigie Kinana. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza kuhusu suala hili."

Kwa upande wake Malima, alisema: "Tuliitwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi. Kwa kuwa tuliitwa kama viongozi wa chama, basi maelezo yote yako kwa Katibu Mkuu wa CCM (Kinana).

Mtafuteni yeye kwa kuwa ndiye msemaji wa chama kwenye suala kama hili."

Mbunge wa zamani wa Mkuranga aliongeza: "Sina hofu yoyote ya kufutwa uanachama kwa sababu sioni sababu ya kufutwa uanachama."

KUNUNUA NDEGE
Bashe amekuwa miongoni mwa wabunge wachache wa CCM ambao wamekuwa wakisimama kwenye vikao vya Bunge la 11 na kukosoa utendaji na baadhi ya maamuzi yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Miongoni mwa mambo ambayo mbunge huyo alisimama na kukosoa bungeni ni uamuzi wa serikali kununua ndege ambao alidai hauna tija akidai kipaumbele cha Watanzania kwa sasa siyo ndege na kwamba serikali inaingia kwenye uwekezaji huo katika kipindi ambacho mashirika mengi ya ndege yanatangaza kupata hasara.

Musukuma alipaa kisiasa nchini wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, tukio kubwa likiwa kutua kwake kwa chopa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa alipokuwa anazindua 'Safari ya Matumaini'.

Musukuma pia 'alitikisa' kwenye mkutano uliopita wa Bunge kwa kupinga njia ya kutaja majina ya wanaojihusisha na dawa za kulevya iliyokuwa inatumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Malima aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Alianguka kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM akizidiwa kura na Mbunge wa sasa wa Mkuranga mkoani Pwani, Abdala Ulega.

No comments:

Post a Comment