Friday, March 17, 2017

HATIMAYE KESI YA LWAKATARE UTATA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imehoji hatima ya kukamilisha upelelezi wa kesi ya kula njama ya kudhuru kwa sumu, dhidi ya Mkurugenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),

Wilfred Lwakatare na mwenzake itajulikana lini kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kutoa taarifa inayoeleweka.

Kesi hiyo ilitajwa juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mwendesha Mashtaka, Hamisi Saidi, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake haujakamilika.

Hakimu alisema upelelezi wa kesi hiyo haijulikani taarifa zake kwamba umefikia wapi kwa sababu kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 20 mwaka 2013, imetajwa mahakamani mara nyingi bila kujulikana hatima yake.

Hata hivyo, mdhamini wa Lwakatare aliitaarifu mahakama kwamba mshtakiwa huyo ni mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 14 mwaka huu na dhamana ya washtakiwa inaendelea.

Katika kesi hiyo, mbali na Lwakatare, mshtakiwa mwingine ni Ludovick Joseph na wanadaiwa kuwa Desemba 28, mwaka 2013 katika eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walikula njama za kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.

No comments:

Post a Comment