Duru za siasa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, zimeanza kutaja chanzo
cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye, kupoteza wadhifa huo.
Vyanzo mbalimbali vinaonesha kuwa vumbi la Uchaguzi Mkuu la Mwaka 2015
bado linaendelea kutimka ndani ya CCM. Baada ya chama hicho kumfukuza
uanachama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM, Sofia Simba, na
wenyeviti watano wa CCM wa Mkoa katika Mkutano Mkuu wa Dharura mwezi
uliopita mjini Dodoma, huku wengine wakipewa onyo, duru zinaonesha kuwa
Nape Nnauye naye kawa mhanga.
Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM, Mbunge wa sasa wa Nzega
(CCM), Hussein Bashe, alipata kumtuhumu Nape hadharani kuwa alikuwa
akishirikiana na Mwenyekiti wa CCM (wakati huo), Jakaya Kikwete, kumbeba
Bernard Membe.
Bashe alimtuhumu Nape kuwa katika kulipwa fadhila, Membe aliahidi
kumwachia Jimbo la Mtama agombee, suala ambalo lilitokea Nape akagombea
na kushinda.
“Pamoja na kazi kubwa aliyofanya Nape kumnadi bwana mkubwa, bado wapo
watu wamepenyeza maneno yaliyodhoofisha uhusiano wao. Mara kadhaa
wamekuwa wakimwambia bwana mkubwa kuwa Nape ni wakala wa Membe ndani ya
Serikali yake. Hili hakulipenda Mhe. Rais Magufuli, hivyo wakawa na
mgogoro wa kimyakimya,” anasema mtoa habari wetu.
Vyanzo vya habari vinasema ushauri alioutoa Membe mara tu baada ya Rais
Magufuli kuingia madarakani na kupiga marufuku safari za nje, Rais
Magufuli hakuupenda. “Tanzania si kisiwa,” alisema Membe wakati huo na
kushauri Serikali isijitenge na jamii ya kimataifa kwa Rais na maafisa
wa Serikali kutosafiri nje ya nchi.
Kinachodaiwa kuwa ni uhusiano wa Nape na Membe kiliongeza msukosuko
baada ya Nape kupingana na kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam alipoamua
kutangaza hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kufanya biashara ya
dawa za kulevya pale Nape aliposema, “Kutangaza majina ya watu bila
ushahidi kunaweza kuharibu heshima na ‘brands’ za wasanii walizotumia
nguvu na muda kuzijenga.”
Nape alitaka watuhumiwa wafikishwe mbele ya vyombo vya dola na
wachunguzwe kisha watakaoonekana wana hatia wafikishwe mbele ya Mahakama
kujibu mashitaka, ila si kutangazwa bila ushahidi kwani mbele ya safari
inaweza kuthibitika hawauzi dawa za kulevya ikawa wameharibiwa heshima.
‘Kutia mafuta kwenye moto unaowaka’, Nape akaunda Kamati kumchunguza
kiongozi kipenzi cha Mhe. Rais, pale kiongozi huyo alipovamia Kituo cha
Radio na TV cha Clouds (CMG). Mkuu wa nchi alikwishasema ‘… chapa kazi.
Usikwazwe na maneno ya mitandaoni.’ Kamati aliyoiteua Nape ikathibitisha
kuwa hayakuwa maneno ya mitandaoni ni kweli kiongozi huyo alivamia
Clouds, hili lilimkera mno Mhe. Rais akaona amtumbue,” kimesema chanzo
chetu.
Gubu la kutoungwa mkono katika mchakato wa kisiasa linaonekana kuisumbua
CCM kitambo sasa. Januari 30, 1984 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa
Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alivuliwa madaraka mjini Dodoma,
alipobainika kuwa alitaka katika uchaguzi wa mwaka 1985 aipe madaraka
zaidi Zanzibar. Hii ya mwaka 1984 ilipewa jina maarufu kama ‘Kuchafuka
kwa Hali ya Hewa Ndani ya CCM’.
Mwaka 1985, Maalim Seif Shariff Hamad alituhumiwa kumhujumu Idris Abdul
Wakil asipate ushindi wa kishindo Zanzibar, na pamoja na kumteua
aendelee na Uwaziri Kiongozi wa Zanzibar, wawili hao waliendelea kuishi
kwa kutoaminiana hadi Januari 26, 1988 wakati Abdul Wakil alipotengua
uteuzi wa Maalim Seif na kumteua Dk. Omar Ali Juma.
Mgogoro uliendelea na ilipofika Mei 1988, Maalim Seif alijiondoa CCM.
Seif aliondoka na akina Shaaban Mloo, Maulid Makame, Ali Haji Pandu na
Hamad Rashid Mohamed. Baadaye kundi hili lilifungwa jela miezi 30 na
liliachiwa baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi ambapo wote hawa
walikwenda kuwa waanzilishi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Mwaka 1995, Augustino Mrema alijiondoa CCM baada ya kutofautiana na
Serikali ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuhusiana na kashfa ya mashamba ya
mkonge Tanga, ambapo mfanyabiashara P. V. Chavda alipokuwa amepewa
mashamba kinyume cha utaratibu. Mrema alijiunga na Chama cha
NCCR-Mageuzi ambapo alileta hamasa kubwa katika uchaguzi mkuu kwa kupata
asilimia 27.7 ya kura zote.
Uchaguzi huo aliogombea na Benjamin Mkapa duru zinaonesha kuwa kama si
nguvu ya Mwalimu Julius Nyerere, ilikuwa Mrema anaingia Ikulu. Ndani ya
CCM yalibaki makovu na wengi walidhani CCM ingesambaratika baada ya
wimbi hilo, ila baadaye ikajikusanya.
Februari 7, 2008, Edward Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu baada ya kuwapo
taarifa za fitina kuwa alikuwa anajiandaa kugombea urais mwaka 2010.
Ilielezwa kuwa Lowassa alikuwa na mkakati wa chini kwa chini
kutenganisha kofia za Mwenyekiti wa CCM na urais, na kwamba Lowassa
angetumia fursa hiyo kumwangusha Rais Kikwete.
Mgogoro huu wa chini kwa chini uliwagawa wafuasi wa viongozi hao ndani
ya CCM, lakini ilipofika mwaka 2010 Lowassa hakujitokeza kugombea ubunge
ikathibitika kuwa ulikuwa uvumi uliopenyezwa na wajanja waliokuwa
wanajitafutia fedha.
Mwaka 2015, Rais Kikwete alipotangaza bayana kuwa Lowassa hawezi
kuteuliwa kuwa mgombea ndani ya CCM na Chama kikampitisha Rais John
Magufuli, Julai 30, mwaka huo Lowassa aliamua kujiondoa CCM na kujiunga
na Chadema. Uamuzi wa Lowassa ulileta changamoto kubwa, hali
iliyopunguza kura za CCM na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi
hii upinzani ukapata kura takribani asilimia 40.
Kutokana na hofu ya mgawanyiko uliotokea mwaka 2005, mwaka huu CCM
imebadili kanuni yake baada ya kuwapo taarifa za chini kwa chini kuwa
walikuwapo wana-CCM waliokuwa wanajipanga kugombea urais mwaka 2020,
ambapo kwa sasa Rais aliyeko madarakani kwa CCM imepitishwa rasmi mwaka
2020 ndiye atakayekuwa mgombea wao.
“Mazingira haya unayoona hadi Rais anajiwekea kinga ya mwaka 2020 ndiyo
yaliyomponza Nape. Wengi wanaamini Membe aliko huko nje ya ulingo wa
siasa anafanya mazoezi ya kugombea urais. Kama vile hiyo haitoshi,
wakubwa wameona wamwondoe hata Nape waliyedhani anawafikishia kila
taarifa. Kwa hiyo, hata kama Nape asingekwaruzana na … bado wakati
ungefika akaondolewa tu kwa nia ya kulinda siri za Serikali,” kimesema
chanzo chetu.
Juhudi za JAMHURI kuthibitisha taarifa hizi kutoka kwa wasaidizi wa
karibu wa Rais hazikuzaa matunda. Hata hivyo, Katibu wa Uenezi na
Itikadi wa CCM, Humphrey Polepole, ameliambia JAMHURI: “Si kweli kabisa.
Wanaosema hivyo, wapuuzwe. Kwanza Nape hakufukuzwa uwaziri, uwaziri
wake haujatenguliwa, bali Rais amefanya mabadiliko madogo katika Baraza
la Mawaziri.”
Polepole amesema si dhambi wakati wa mchakato ndani ya chama kila mtu
kuwa na mgombea anayempenda, ila baada ya mchakato kukamilika
anayeteuliwa anakuwa mgombea wa wanachama wote. “Huo ndiyo utaratibu wa
CCM. Baada ya mchakato tunavunja makundi. Hivyo aliyesema hivyo si
mkweli. Apuuzwe.”
JAMHURI limemtafuta Nape kuzungumzia sakata la kufukuzwa kwake, akasema:
“Kaka naomba mniache nipumzike kwa sasa. Maneno niliyokuwa nayo
niliyasema siku hiyo mbele ya wanahabari. Nimesema bayana kuwa naunga
mkono juhudi za Rais wangu kujenga nchi yetu. Sina kinyongo na Rais
wangu. Nampongeza kwa uteuzi alioufanya na nitaendelea kuwa mwanachama
mtiifu kwa nchi yangu na CCM.
“Nimesema mimi ni mbunge na namshukuru Mhe. Rais kwa kunipa nafasi ya
kutumikia uwaziri. Wapo wabunge wengi, hawakuteuliwa kushika wadhifa
huo, na hawakuhoji nilipoteuliwa mimi. Vivyo hivyo, umefika wakati wa
Mtanzania mwingine kushika wadhifa huo, mimi sina kinyongo kabisa.
Naunga mkono hatua hii. Niache nipumzike kidogo nitumikie wananchi wa
jimbo langu la Mtama. Nawashukuru wanahabari na Watanzania kwa kuendelea
kunipa moyo.”
Nape amekuwa ni miongoni mwa vijana wachache wa CCM ambao waliaminiwa na
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, baada ya
kutumikia nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, wilaya
ambayo ni nyumbani kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa,
alipata nafasi kubwa.
Nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliipata baada ya kupitia
katika tanuri kipindi hicho akiwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada
ya kuwashambulia baadhi ya makada aliowatuhumu kuingia mkataba wa ujenzi
wa jengo katika kiwanja cha Umoja huo kilichopo makutano ya barabara za
Lumumba na Morogoro.
Nape alichukua nafasi baada ya kuachwa wazi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora wa
sasa, Aggrey Mwanri, ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Siha, mkoani
Kilimanjaro. Ni kipindi ambacho Nape, pamoja na watumishi wengine wa
Sekretarieti ya CCM, walikichukua chama kikiwa kimezongwa na tuhuma za
ufisadi zilizokuwa zinawakabili wanachama wake.
Katika harakati za kukisafisha chama na kukirejesha kwenye mstari,
alipata fursa ya kuzunguka sehemu kubwa ya nchi kukinadi CCM.
Atakumbukwa kwa aina yake ya kuishambulia Serikali, hasa pale wananchi
walipoonekana kutoa lawama kwa baadhi ya mawaziri.
Katika harakati hizo za kukijenga CCM, yaliibuka majina kama vile
“mawaziri mizigo”, huku ujumbe huo ukiwa maarufu katika majukwaa ya
siasa.
Ndani ya CCM, ambako leo Nape si miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu wala
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, nafasi ambazo alikuwa akiingia kwenye
vikao kwa nafasi yake, leo hana nafasi hiyo tena.
Lakini mbali na kutokuwa kwenye nafasi hiyo tena, CCM kina jambo lolote
la kujifunza kutoka kwa aliyekuwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi? Jibu
ni rahisi sana, ndiyo. Hakuna anayeweza kubisha kwamba baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2010, CCM haikuwa inatamanika tena, wananchi wakapoteza
matumaini.
Chama hicho kilipoteza mvuto zaidi baada ya kuingia mikononi mwa Wilson
Mkama, msomi mzuri, ambaye alitarajiwa kuleta mageuzi makubwa ndani ya
CCM, hasa kupitia mkakati wa kujivua gamba.
Chombo kilipoonekana kwenda mrama, Nape alichukua unahodha na
kukiendesha kwa ustadi mkubwa. Mwenyekiti wa wakati huo na Rais wa Awamu
ya Nne, Jakaya Kikwete, aliamua kumkumbuka rafiki yake wa muda mrefu,
tangu wakiwa jeshini Abdulrahman Kinana, huku nafasi ya Itikadi na
Uenezi akikabidhiwa kwa kijana mdogo wakati huo Nape akiwa na miaka 34
tu.
Hapo ndipo inapokuja historia ya kulala porini kwa siku zaidi ya 850,
akijaribu kukijengea taswira mpya chama chake kwa wanachama. Jambo hilo
amelisema hata baada ya kutishiwa bastola, akisema “Wakati ninahangaika
na chama hiki, ninyi mlikuwa mnakunywa bia tu… nimezunguka nchi hii
miezi 28, nikijenga chama changu CCM.”
No comments:
Post a Comment