Tuesday, February 7, 2017

WALIMU WATANGAZA KUGOMA MWEZI UJAO



CHAMA cha Walimu Tanzania  (CWT), kimetangaza mgogoro na serikali endapo haitalipa madai yao zaidi ya Sh. bilioni 800 kabla ya Machi mosi, mwaka huu.

Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba, aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu maazimio ya Baraza la Taifa la CWT.

 “Ikiwa serikali haitatekeleza hoja zote zilizotolewa na CWT, tutatangaza mgogoro kati yetu na serikali kuanzia Machi mosi, mwaka huu bila ya notisi nyingine kutolewa,’’ alisema.

Alisema Baraza la Taifa la CWT, linatarajia kuwa serikali itatumia mwezi wa pili kulipa madeni yote ya walimu na kutatua kero zao ili kuepuka mgogoro usio wa lazima kati yake ambaye ni mwajiri wao na walimu.

Alisema (CWT) iko tayari kwa majadiliano na serikali juu ya mkakati wa kutekeleza matakwa hayo.

Aidha, Mukoba alisema Baraza la Taifa lilikaa mwishoni mwa mwezi uliopita mkoani Morogoro kutaka kujua hatua zilizochukuliwa na serikali kutatua kero mbalimbali za walimu ikiwa ni pamoja na kulipa madeni yao.

Alisema vilevile, Baraza la Taifa  lilijulishwa  kuwa takribani walimu 182,000 wamelipwa jumla ya Sh. bilioni 124 kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/14 hadi Desemba, 2016.

 “Chama kinapongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali. Hata hivyo, kiasi kilicholipwa ni kidogo ukilinganisha na madeni halisi ya walimu,” alisema Mukoba.

Alisema baada ya (CWT) kuchukua hatua hizo za kuhakikisha kuwa walimu wanalipwa madeni yao na serikali kulipa sehemu ndogo ya madai yao, Baraza la Taifa lilibaini kuwa madeni ya walimu yanazidi kukua kwa kasi kiasi kwamba hatua za haraka zisipochukuliwa, hayatalipika.

Mukoba alitaja baadhi ya matatizo ya walimu yanayopaswa kutatuliwa na serikali ni pamoja na kulipa walimu 80,000 waliopandishwa madaraja kati ya Januari na Aprili, 2016 ambao hawajarekebishiwa mishahara yao na kulipwa mapunjo yao yaliyofikia takribani miezi 12.

 Alisema chama kinakadiria kuwa takribani Sh. bilioni 300 zinahitajika kuwalipa walimu stahili inayohusiana na kupandishwa madaraja, walimu 39,000 wanaopaswa kupandishwa madaraja katika mwaka wa fedha kuanzia Julai 2016.

Alisema pia mkataba wa walimu na serikali unaelekeza kuwa ikiwa serikali haijaongeza mishahara kama ilivyofanya katika mwaka huu wa fedha, walimu wanapaswa kuwa na nyongeza ya mwaka kuanzia Julai mosi, mwaka jana, ambayo ni tarehe ya kuanza kwa mwaka huu wa fedha.

Mukoba alisema madai yasiyohusiana na mishahara yaliyowasilishwa serikalini yanafikia Sh. bilioni 26.4 na bado hayajalipwa na walimu waliostahili kulipwa fedha za likizo hawakupewa.

“Walimu wastaafu 6,044 hawajalipwa mafao yao ya kustaafu yanayokadiriwa kufikia Sh. bilioni 480 kabla ya kuongeza tozo ya asilimia 15 na kikwazo kikubwa katika kuwalipa stahili zao ni serikali kudai kuwa bado wanahakiki wafanyakazi hewa na vyeti,” alisema.

Hata hivyo, alisema Baraza la Taifa linaungana na serikali katika hatua zilizochukuliwa za kuhakiki vyeti na wafanyakazi hewa.

 “Isipokuwa linatambua kuwa kazi hii imeingia mwezi wa saba mpaka sasa na Baraza linatoa rai kuwa uhakiki huo usitumiwe kama njia ya kuzuia kulipa madeni ya walimu,” alisema.

No comments:

Post a Comment