Wabunge waliohojiwa mjini Dodoma jana, walisema kinachoendelea ni siasa badala ya uhalisia.
Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT – Wazalendo), Zitto Kabwe alisema kinachoendelea ni siasa za kuchafuana na kwamba Makonda ajiandae kubeba msalaba wake katika jambo hilo.
“Juzi hapa nililalamika bungeni kwamba leo wanakamatwa wasanii, kesho watakamatwa wabunge. Mmeona leo Makonda amemtaja Mbowe. Kinachoendelea ni siasa za kuchafuana. Kitendo cha Makonda kumtaja Mbowe maana yake ni kwamba kazi anayoifanya si yake, ni kazi ambayo ametumwa na wakubwa wake na ndiyo maana wanamuunga mkono,” alisema.
Zitto aliwataka wabunge wa upinzani bila kujali tofauti zao za vyama, kuliona suala la Mbowe kuwa si shambulio kwa mbunge huyo wa Hai pekee yake, bali ni mashambulizi dhidi ya wabunge wa upinzani. “Tukiliacha bila kulisemea maana yake kesho na keshokutwa kila mbunge wa upinzani anaweza kuonekana ni muuza dawa”.
Hata hivyo, Mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu alisema anaamini hadi Makonda kuamua kumtaja Mbowe na watu wengine, atakuwa na ushahidi kwa sababu hawezi kufanya hivyo pasipo ushahidi. Balozi Adadi ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), alisema anaamini kabla ya kutangaza majina hayo, aliwasiliana na Jeshi la Polisi kwanza.
Lakini Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema wameamua kumchukulia Makonda kama mtu anayetumwa, huku akisema Jeshi la Polisi limemwachia mkuu huyo majukumu yake.
No comments:
Post a Comment