Mvutano
umeibuka bungeni kati ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman
Mbowe na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson baada ya Mbunge huyo wa Hai
kumwuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa swali lililopingwa na Naibu Spika
kwa maelezo kuwa ni la kisheria si la kisera.
Sakata
hilo liliibuka asubuhi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu,
baada ya Mbowe kuhoji sababu za Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kusota rumande kwa kukosa dhamana, Peter Lijualikali wa Kilombero
anayetumikia kifungo cha miezi sita gerezani na wanachama wengine wa
Chadema wanaokabiliwa na mashitaka mbalimbali.
Mbowe
alimtaka kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni, aeleze kama ni
sera ya Serikali kuua vyama vya upinzani, huku akisema Rais John
Magufuli alipata kutamka kuwa atavimaliza vyama vya upinzani kabla ya
mwaka 2020.
Kwa maswali hayo, Dk Tulia alimtaka Waziri Mkuu kujibu swali linalohusu sera na kuachana na yanayogusa masuala ya kisheria.
Jambo
hilo liliwafanya wabunge wa Upinzani huku wakipiga meza kwa takribani
dakika tano kupinga, wakimtaka Naibu Spika aache Waziri Mkuu ajibu swali
hilo.
Katika
swali lake la msingi, Mbowe alisema wakati jana ikiwa ni Siku ya Haki
Duniani, imepita miezi mitatu tangu Lema aanze kusota rumande huku
akinyimwa dhamana licha ya kuwa iko wazi.
Pia
alisema Lijualikali anatumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la
kisiasa sambamba na mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa wa Lindi, Suleiman
Mathew aliyefungwa miezi minane na madiwani zaidi ya sita na viongozi
wengine 215 nao wakifungwa au kuendelea na mashitaka huku zikifanyika
hila za kuidhoofisha CUF.
“Haya
yanayoendelea katika Serikali ambayo ni kinyume na utamaduni na mazoea
yetu kama Taifa, je ni utekelezaji wa sera ya kuua upinzani chini ya
Rais Magufuli?” Alihoji Mbowe.
Kabla ya Waziri Mkuu kujibu swali hilo, Dk Tulia aliingilia kati na hali kuwa hivi:
Dk Tulia:
Katika swali lako kuna masuala ya kisera na kisheria. Maswali
yanayomhusu Lema na Lijualikali na madiwani sita ni ya kisheria, hayo
kuhusu leo (jana) kuwa siku ya haki duniani, Waziri Mkuu anaweza
kuyajibu.
Majaliwa: Nakanusha,
Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani, nchi inaongozwa
kwa sheria, kanuni na taratibu na kuna Bunge, Serikali na Mahakama.
Hakuna mhimili unaoingilia mhimili mwingine. Jambo lililopo mahakamani
halizungumzwi kokote, siwezi kuzungumzia hilo.
Mbowe:
Kwa kuwa Rais anaonekana kuvunja Katiba ikiwa ni pamoja na kupiga
marufuku mikutano ya vyama vya siasa, je tukileta ushahidi kuwa Rais
amekusudia kuumaliza upinzani kabla ya 2020, Waziri Mkuu utakuwa tayari
kuwajibika kwa kujiuzulu?
Dk Tulia:
Mbowe swali lako la maelezo ya jumla, yako sawasawa ila la kumtaka
Waziri Mkuu kuwajibika si la kisera, kuwajibika si sera uliza swali la
kisera.
Mbowe: Labda
swali langu nilielekeze kwa Naibu Spika (Dk Tulia). Swali langu
lilikuwa la mwendelezo ambalo hutokana na majibu ya msingi yaliyotokea.
Kama kulikuwa na msingi wa kisera kwenye swali la msingi, swali la
mwendelezo linakwenda kutokana na majibu yaliyotolewa. Waziri Mkuu aseme
tu kama yupo tayari kujiuzulu tukileta ushahidi.
Katika
maelezo yake, Dk Tulia alitaka Mbowe ajikite katika swali la kisera
jambo ambalo Mwenyekiti huyo wa Chadema alipinga na kusisitiza kuwa
huenda mambo yanayofanyiwa wapinzani, wabunge, mawaziri Serikali
inayafurahia.
No comments:
Post a Comment