Aliyekuwa
Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa,
amewasilisha barua mahakamani akiomba kuondoa kesi aliyoifungua
akipinga kustaafishwa kwa nguvu ili wakamalizane katika nyumba ya
maaskofu.
Mokiwa
anataka kuondoa kesi hiyo ya madai namba 20 ya mwaka huu aliyofungua
dhidi ya Askofu Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk.
Jacobe Chimeledya na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo.
Askofu Mokiwa alifungua kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Akiieleza
mahakama, Wakili wa wadaiwa, Gabrieli Masinga alidai alipokea barua
kutoka kwa Wakili wa Askofu Mokiwa, Wakili M.B. Kabunga ikiwaelekeza
kuwa kesi iliitwa jana kwa sababu waliwasilisha barua ya kuomba kuiondoa
mahakamani.
Alidai barua hiyo ilieleza sababu za kuondoa kesi hiyo ni kutokana na juhudi za kutatua mgogoro huo katika nyumba ya maaskofu.
“Wanaomba kuondoa kesi wapate muda wa kujadiliana kwa sababu juhudi haziwezi kufanyika bila kesi hiyo kuondolewa mahakamani,”alidai.
Hakimu Simba alisema barua hiyo hajaiona na kesi hiyo ilipangwa Februari 28 hivyo kuwapo kwao jana mahakama hakutambui.
“Leo
mliitwa na nani, mimi siandiki kitu, niandike ili iweje, siwahitaji,
kesi imepangwa tarehe 28, pisheni wengine waendelee. Naona kuna barua
ya kumalizana katika nyumba ya maaskofu, kama ni hivyo nawaombea
usuluhishi mwema,”alisema Hakimu Simba.
Askofu
Mokiwa na wakili wake wote hawakufika mahakamani. Hata hivyo Wakili
Masinga alidai askofu huyo anataka kurejeshewa uaskofu wake, anaomba
mahakama itengue uamuzi wa kumstaafisha kwa nguvu.
“Mokiwa
alivuliwa uaskofu wake na Januari 7 mwaka huu akakimbilia mahakamani,
mambo yanayohusu imani yanatakiwa kushughulikiwa katika nyumba za imani.
“Huwezi
kuvuliwa madaraka msikitini ama kanisani ukakimbilia mahakamani,
masuala hayo yanajadiliwa katika vyombo husika labda pakiwapo ukiukwaji
wa sheria za nchi,”alidai.
Kwa
mujibu wa barua kwa mapadri na maaskofu wote wa Kanisa la Anglikana
Jimbo la Dar es Salaam, kiongozi huyo alilazimishwa kuvuliwa uaskofu
Januari 7 mwaka huu.
Sababu
za kuvuliwa madaraka kwa kiongozi huyo wa muda mrefu wa kanisa hilo ni
kudaiwa kuhusika na ufujaji wa mali za kanisa na matumizi mabaya ya
madaraka.
Inadaiwa
katika hati kwamba hatua hiyo inatokana na mashtaka yaliyowasilishwa
dhidi yake na wadhamini wa makanisa mbalimbali ya Jimbo la Dar es
Salaam, ambayo ni Yombo Buza na Magomeni ambao walilalamikia matumizi
mabaya ya madaraka kwa kile walichoita ufisadi huku wakimtaka aandike
barua mwenyewe ya kujiuzulu lakini aligoma kufanya hivyo.
Mokiwa
anakabiliwa na mashtaka 10 huku shtaka la tatu la uwekezaji, ndilo
lililomtia hatiani na yeye kukiri kosa mbele ya tume hiyo ya uchunguzi.
Kesi
hiyo itaendelea Februari 28 mwaka huu na mahakama itaelezwa kama kuna
makubaliano ya kuondoa kesi wakamalizane nje ya mahakama au la.

No comments:
Post a Comment