Monday, June 11, 2018

MKWASA AFUNGUKA YANGA INAWACHEZAJI SABA TU


BAADA ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kusema sababu za Yanga kujitoa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame mwaka huu hazina mashiko uongozi wa klabu hiyo umesema hawana wachezaji wa kuunda timu ambayo itaenda kuchuana kwenye michuano hiyo.

Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu, Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, alisema kwa sasa timu yao imebakiza wachezaji saba tu wenye mikataba na waliobakia wako huru.

Mkwasa alisema klabu kwa sasa imeanza mazungumzo na wachezaji wengine kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao huku akiiambia TFF kuwa nyota wake hao waliobakia wamekwenda mapumziko.

"Sisi hatuna timu, tumebakia na wachezaji saba tu, wengine wamemaliza mikataba na huwezi kuwalazimisha kucheza, na wale wa U-20 wameenda Dodoma katika michuano ya vijana, wangekuwapo tungewaunganisha wakaenda kucheza, sasa wanataka tupeleke nini," alisema Mkwasa.

Rais wa TFF, Wallace Karia, aliiambia Yanga inapaswa kubadilisha uamuzi wao kwa sababu michuano hiyo pia itawasaidia kuwaimarisha kuelekea katika mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Kadhalika, Karia alikosoa sababu iliyotolewa na Yanga kuwa ratiba ya mechi za kimataifa imewabana jambo ambalo kwa sasa klabu hiyo imekuja na suala la wachezaji kumaliza mikataba.

“Bado hatujaitaarifu Cecafa (Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati) kuhusu kujitoa kwa Yanga, kwani sababu walizozitoa juu ya kutoshiriki michuano ya Kagame hazina mashiko.

"Si Yanga peke yao ambao ratiba imewabana na ukiangalia michuano hiyo ya Caf (Kombe la Shirikisho Afrika) hata Gor Mahia pia wapo, lakini pia wanashiriki hadi sasa mashindano ya SportsPesa Super Cup (walicheza fainali jana)dhidi ya Simba," alisema Karia kabla ya Yanga kukutana jana na Mkwasa kutoa kauli hiyo.

Katika mashindano ya Kombe la Kagame ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu, Yanga ilipangwa Kundi C pamoja na Simba, St.George (Ethiopia) na Dakadaha kutoka Somalia.

Bado Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) halijatoa uamuzi wowote baada ya Yanga kutangaza kujitoa kwenye michuano hiyo ambayo bingwa wake anapata zawadi ya Dola za Marekani 30,000.

Timu nyingine za Tanzania zilizobakia katika mashindano hayo ni bingwa mtetezi, Azam FC na Simba zote za jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment