KATIKA mwendelezo wa kufufua viwanda nchini, serikali iko katika mchakato wa kuviuza viwanda 12 vilivyo ‘hoi bin taabani’, ili viendelezwe na watu wenye uwezo.
Viwanda hivyo ni miongoni mwa 56 ambavyo vimekufa na kushindwa kuzalisha, kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa na serikali miaka 15 iliyopita.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alisema hayo jijini Dar es Salaam kuwa kati ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, 62 ndivyo vinafanya kazi vizuri, viwanda 10 havikubinafsishwa ila mali zake zilisambazwa na viwanda 56 vimefungwa na havifanyi kazi. Pia alisema viwanda 28 vinafanya kazi kwa kusuasua na 12 vimekufa kabisa.
Dk. Meru alisema viwanda 12 ambavyo vimekufa, Serikali inatarajia kuvitangaza kwa lengo la wenye uwezo wavichukue na kuviendeleza na kwamba imeshavitembelea viwanda hivyo na kuviona, kisha kuwauliza wamiliki wake kama wana mpango wowote wa kuviendeleza, lakini hawakuwa na majibu yoyote.
Dk. Meru alisema miaka 15 iliyopita Tanzania ilibinafsisha viwanda 156 kwa lengo la wawekezaji kuviendeleza na baada ya kuvitembelea viwanda hivyo, wengi wao wamevifunga, wengine wamebadilisha matumizi, huku wengine wakivigeuza kuwa mabwalo.
Alisema kwa sasa serikali inachokifanya hainyang’anyi mtu kiwanda bali kama kimeshindwa kuendelezwa anapewa Mtanzania
mwingine mwenye uwezo.
Kuhusu hali ya uwekezaji katika viwanda, Dk. Meru alisema inaendelea vizuri na kwamba wawekezaji wanaendelea kuja nchini na kuwekeza.
Alisema awali kulikuwa na tatizo la upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kwamba wawekezaji waliokuwa wanakuja na kukosa sehemu ya kuwekeza.
“Sasa hivi serikali imeanza mkakati wa kuwaimiza wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda,” alisema.
“Kwa sasa maeneo hayo yameshatengwa kupitia taasisi mbili za uwekezaji ambazo ni EPZA (Mamlaka ya Maeneo ya Uwekezaji) na Taasisi ya Uwekezaji (TIC),” alisema.
No comments:
Post a Comment