Benchi la ufundi la timu hiyo limeeleza sababu zilizomfanya kushindwa kufurukuta.
Akizungumza na Nipashe, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema sababu za Tshishimbi kutoonyesha makali yake kwenye mchezo wa juzi ni kutokana na kukamiwa.
Alisema katika mchezo huo dhidi ya Lipuli, Tshishimbi alitimiza majukumu yake, lakini alikuwa amepaniwa na viungo wa Lipuli ambao walikuwa wakizunguka naye kila kona ya Uwanja.
“Mimi naona amecheza vizuri na ametimiza majukumu yake, labda niseme tu hakuwa na uhuru kutokana na wenzetu (Lipuli) kuweka watu maalum ambao walikuwa wakicheza naye kila eneo,” alisema Nsajigwa.
Alisema kiungo huyo anaendelea kuizoea ligi na atakuwa na mchango mkubwa atakapoizoea vizuri.
Aidha, Nsajigwa alisema benchi la ufundi la Yanga limewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na hofu na timu yao kufuatia matokeo hayo.
Nsajigwa, alisema matokeo waliyoyapata kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Uhuru ni ya kawaida na mashabiki hawapaswi kuumia.
Alisema matokeo hayo yametokana na ugumu wa mchezo huo hasa mbinu walizokuwa wakitumia wapinzani wao katika kupoozesha mechi.
“Mchezo ule ulikuwa mgumu, wenzetu walikuja kwa lengo la kupata sare, walikuwa wanapoteza muda kwa kujiangusha ovyo, lakini pia walicheza kwa kutukamia,” alisema nahodha huyo wa zamani wa timu hiyo.
Alisema mchezo huo umepita na sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo ujao wa ugenini dhidi ya Majimaji ya Songea utakaochezwa Septemba 9, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment