Monday, July 31, 2017

SERIKALI YABAINI WAKIMBIZI "FEKI"

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Idara ya Uhamiaji, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, kuhakikisha inaimarisha ulinzi katika mipaka yake ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa wingi kukimbia njaa kwenye nchi zao.

Aidha, alisema serikali imebaini kuwapo kwa wingi wa wakimbizi ‘feki’ wanaoingia nchini kwa kisingizio cha kukimbia vita ilhali ukweli ni kwamba wanakwepa njaa, hivyo kuigeuza Tanzania kuwa lango la kuwafadhili. 

Majaliwa alionyesha wasiwasi wake huo na kutoa maelekezo juu ya nini  cha kufanya wakati akizungumza na watumishi wa mpaka wa Kasumulu unaotenganisha Tanzania na Malawi.

Akizungumzia hatari ya ujio huo wa wahamiaji haramu nchini, Majaliwa alisema pasipokuwa na udhibiti, wageni hao wanaweza kusababisha ongezeko la watu nchini, hivyo kuathiri mipango ya maendeleo.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa, wilaya na uhamiaji, hakikisheni wakimbizi wanaoingia nchini ni wale tu ambao nchi zao zina vita. Kumekuwapo na wimbi la watu wanaoingia nchini wakikimbia njaa kwenye nchi zao. Naomba hili mliangalie. Watanzania tuko zaidi ya milioni 50 sasa…  kama mtawaruhusu hawa tutajikuta tunafika watu milioni 60,” alisema Majaliwa.

Pia, alisema kumekuwapo na wimbi la ungiaji wa silaha za kivita ambazo hazijawahi kuwapo nchini, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

“Tanzania tunaishi kwa amani na utulivu. Hivyo wahalifu wanaotoka nchi za jirani wasifanye hapa ni jumba la kupumzikia. Vyombo vya ulinzi na usalama shirikianeni kuimarisha ulinzi,” alisema, huku akisisitiza kuwa tahadhari hiyo ichukuliwe zaidi katika maeneo yenye njia ziitwazo za panya.

Aidha, Majaliwa aliipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka huo, kwa kukusanya kodi kwa zaidi ya asilimia 100 ya malengo waliyojiwekea kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alisema katika kipindi cha mwaka 2016/ 17 walikamata wahamiaji haramu 87 wakiwamo raia kutoka Somalia, Ethiopia na Msumbiji na Mtanzania mmoja ambaye wamekuwa akiwasafirisha.

Makalla alisema katika mpaka huo kuna jumla ya njia za panya 32 ambazo zimekuwa changamoto ya kukabiliana na wimbi hilo la wahamiaji haramu.

Alisema mbali na changamoto hiyo, wahamiaji haramu wamekuwa wakipata shida kuvuka kwenye mpaka huo kwa sababu ya kuwapo ulinzi wa kutosha.

No comments:

Post a Comment