Bendera ya CCM
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Samwel Kiboye amesema Watanzania wote walioshirikiana na kampuni za uchimbaji wa madini ya Acacia, kufanikisha utoroshaji wa madini wakiwamo baadhi ya wenyeviti, madiwani na watumishi wa Serikali, wachukuliwe hatua kali ikiwa ni pamoja na kuchapwa viboko.
Kiboye maarufu kama ‘Namba Tatu’ alisema hayo katika mazungumzo na HabariLeo kwa simu, yaliyofanyika jana. Alisema anakumbuka kauli ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliyepinga vikali rushwa, akisema, katika siku za nyuma, wote walioshiriki rushwa walipobainika, walifungwa jela na kuchapwa viboko ili wajutie zaidi makosa yao.
“Nyerere alisema watu kama hawa walichapwa viboko 12 wakati wanaingia gerezani na viboko 12 wakati wanatoka ili wakamwoneshe wake zao ili liwe fundisho kwa wengine,” alisema Kiboye akimnukuu Nyerere.
Juzi Kamati maalumu ya pili ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu mchanga wa madini, unaosafirishwa nje ya nchi, iliwasilisha ripoti kwa Rais John Magufuli iliyobainisha kuwa kupitia mikataba michafu, Tanzania imepoteza takriban Sh trilioni 108 katika kipindi cha miaka 19 tangu mwaka 1998 hadi 2017 kupitia usafirishaji wa makinikia maarufu kama mchanga wa dhahabu.
Kampuni ya Acacia ilihusishwa na hasara hiyo. Acacia inaendesha shughuli zake katika migodi mitatu nchini Tanzania ya Bulyanhulu na Buzwagi mkoani Shinyanga na North Mara uliopo wilayani Tarime mkoa wa Mara.
“Ukiangalia vizuri, baadhi ya viongozi tangu katika vijiji, kata na hata wilaya, idara na wizara mbalimbali; pamoja na baadhi ya wanasiasa wanaowatetea makampuni kama Acacia ambayo uchunguzi wa kamati mbili zote umebainisha walikuwa wakipora na kuwaibia maskini Watanzania, utaona kuna sura nyingi na kubwa za rushwa na usaliti ndani yake, hao wanastahili viboko,” alisema Kiboye.
Akaongeza, “Kama kuna aliyesaidia hawa wazungu (Acacia) kufanikisha kuwanyanyasa na kuwaibia Watanzania na anayewatetea, basi huyo si mwenzetu, achukuliwe hatua, awe ni mtu wa Serikali, mwanasiasa wa chama chochote au hata nani, huyo si mwenzetu ni msaliti.”
“Rais anawafanyia Watanzania mambo makubwa, Watanzania hawakuzoea sana kwamba kamati zinaundwa, ripoti zinasomwa hadharani na hatua zinachukuliwa. Huyu Rais ni jasiri na mzalendo sijawahi kuona; huyu anastahili pongezi, kuungwa mkono na kuombewa na wote wenye nia njema nchini,” alisema Kiboye.
Akaongeza, “kwa kweli tumeshangaa sana Acacia kufanya kazi bila kibali wala mkataba sahihi.” Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Tarime mkoani humo, Bogomba Rashid alimpongeza Rais Magufuli kwa kuunda kamati mbili tofauti, kuziamini na kuziheshimu kwa kupokea ripoti na kuahidi kwa dhati kuzifanyia kazi.
Bogomba ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kemambo wilayani Tarime akasema, “Kutokana na ripoti hiyo, tunamuunga mkono Rais maana amefanya kazi kubwa kwa Watanzania.
Kabla ya utafiti huu kulikuwa na mambo mengi makubwa yamejificha nyuma ya pazia ambayo Watanzania wengi tulikuwav hatuyaoni wala kuyajua , Kamati hizi za Rais zimetufumbua macho.” Akaongeza, “Kwa kweli ukiacha misimamo au harakati za vyama zisizo na tija, wengi tunaunga mkono maana tukilipwa hizo pesa, Tanzania tutasimama na kujitegemea kiuchumi.”
No comments:
Post a Comment