Mhagama alisema hayo juzi wakati alipotembelea kiwanda cha kusindika nyama cha Nguru Hills Ranch kilichoko wilayani Mvomero, mkoa wa Morogoro. Alisema uwekezaji katika viwanda utaongeza kiwango cha asilimia ya Watanzania watakaojiunga na mifuko ya hifadhi za jamii na kufanikisha kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira ambacho kwa sasa kimeshuka kutoka asilimia13 hadi kufikia asilimia 10.3.
Waziri Mhagama aliambatana na Naibu wake, Anthony Mavunde na kupokewa kiwandani hapo na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro ukiongozwa na mkuu wa mkoa huo, Dk Kebwe Stephen ambaye alifuatana na mkuu wa wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly na watendaji wengine wa serikali ya wilaya na mkoa wakiwemo viongozi wa Kijiji cha Wami Sokoine. Hata hivyo, alisema ziara hiyo ililenga kufuatilia maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara mkoani Morogoro, Agosti 3, mwaka 2016 na kukitembelea kiwanda hicho ambapo moja ya changamoto iliyojitokeza ni ukosefu wa fedha za ukamilishaji kabla ya kuanza uzalishaji wake.
Alisema kutokana na mazungumzo yaliyofanyika mapema mwaka huu, Mfuko wa Pensheni wa LAPF umefikia uamuzi kutoa fedha za kuwekeza kwenye kiwanda hicho ili kumalizika kazi zilizobaki na kukiwezesha kufanya kazi za uchinjaii wa ng’ombe na mbuzi ikiwa na kutoa ajira kwa wananchi miezi sita ijayo mwaka huu. Waziri Mhagama alisema kuwa, Mfuko wa LAPF utawekeza fedha katika kiwanda hicho kulingana na utaratibu wa kisheria utakaosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuona fedha za wanachama zinaingizwa kwenye uwekezaji ulio salama na wenye kuleta faida kwa mfuko na serikali.
Hata hivyo, waziri huyo alisema kuwepo kwa kiwanda cha kuchakata nyama wilayani Mvomero mkoani Morogoro kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wafugaji watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani hapo na wakulima kuzalisha nyasi za malisho. Kwa upande wake Mkurugenzi na Mshauri wa Kiwanda cha Nguru Hills Ranch, Dunstan Mrutu alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 300, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku kutokana na uwezeshaji wa fedha kutoka LAPF kitatarajiwa kufunguliwa ndani ya miezi sita ijayo mwaka huu.
Mkurugenzi huyo alisema takriban asilimia 80 ya nyama itakayochinjwa kiwandani hapo itafungashwa na kuuzwa nje ya nchi, hasa Uarabuni kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania imebainika kuwa na mvuto maalumu katika nchi hizo. Alisema nia yao ni kuitikia mwito wa Rais John Magufuli wa kutaka viwanda vizalishe viatu nchini kuanzia vya majeshi na wananchi wote ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza kuuza bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment