Jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka
aliwaambia waandishi wa habari kwamba shirika lake linadai wateja hao
jumla ya Sh275 bilioni.
“Tunadai kiasi kikubwa sana cha fedha kutoka kwa
wateja wakubwa na wadogowadogo, mpaka Zeco, hivyo tunatoa notisi ya
siku 14 kuanzia leo (jana) walipe deni lao kwani baada ya hapo
tutasitisha huduma pamoja na kuchukua hatua nyingine za kisheria,”
alisema Dk Mwinuka.
Katika kiasi hicho, Zeco inadaiwa Sh127 bilioni
ambacho ni sawa na asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa
mwaka 2016/17 ambayo ni Sh841.5 bilioni.
Pia kiasi hicho ni kikubwa
karibu mara nne ya kile kilichotengwa katika bajeti hiyo kwa ajili ya
mikopo ya ndani ambacho ni Sh33.0 bilioni hali inayoonyesha kwamba Zeco
na SMZ watalazimika kuandaa mpango mkakati wa kulipa deni hilo ambao
utamaanisha kujifunga mkanda ili kulimaliza.
Alipoulizwa kuhusu notisi
hiyo ya kulipa deni, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wa
Zanzibar, Salama Aboud Talib ambaye alikuwa ziarani Pemba alisema hadi
jana hakuwa amepokea barua kutoka Tanesco hivyo asingeweza kuzungumza
chochote.
Wiki iliyopita, akiweka jiwe la msingi katika kituo cha kupoza
umeme cha njia ya Kv 132 mkoani Mtwara, Rais John Magufuli aliiagiza
Tanesco kuwakatia umeme wadaiwa wote sugu ikiwamo Zanzibar.
Alisema
shirikia hilo halipo kisiasa, hivyo wadaiwa wote wakatiwe umeme.
Sambamba na hayo, alilitaka shirika hilo kutoingia mikataba na kampuni
zinazoweza kusababisha au kuongeza madeni, badala yake mwekezaji
yeyote akitaka kuwekeza azalishe umeme wake na kuuza mwenyewe.
Wadaiwa
wengine
Kuhusu wadaiwa wengine, Dk Mwinuka alisema hadi kufikia Januari,
shirika hilo lilikuwa linazidai wizara na taasisi za Serikali kiasi cha
Sh52 bilioni huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa jumla ya
Sh94 bilioni.
Alisema malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha
jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya
shirika kwa wakati ikiwamo uendeshaji, matengenezo ya miundombinu pamoja
na miradi mbalimbali.
Alisema kulipwa kwa malimbikizo hayo ya madeni
kutaisaidia Tanesco kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi zaidi, hivyo
kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea
nishati ya umeme nchini.
Alipoulizwa kuhusu mashirika na taasisi za umma
zinazodaiwa malimbikizo hayo ambayo Tanesco haikuyataja, Msemaji wa
Serikali, Dk Hassan Abbas alisema mashirika hayo yanatakiwa kuanza
kutekeleza agizo hilo kwa kulipa deni kama wanavyodaiwa.
No comments:
Post a Comment