Friday, February 3, 2017

SAKATA LA FEDHA ZA TETEMEKO LAIBUKA BUNGENI


NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA WALEMAVU, ANTHONY MAVUNDE.

SAKATA la fedha za waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mwaka jana mkoani Kagera, limeibuliwa tena bungeni huku serikali ikisisitiza fedha zote zimetumika kwa manufaa ya wananchi, ikiwamo ujenzi wa shule na zahanati.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Anthony Mavunde, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare.

Lwakatare alitaka kujua serikali inachukua hatua gani kuhakikisha fedha zilizotolewa kama msaada kwa waathirika, zikiwamo za wabunge zinawafikia waathirika wa tetemeko hilo mkoani Kagera.

Akijibu swali hilo, Mavunde alisema hata wakirejea katika kumbukumbu rasmi za bunge, Lwakatare ataona kuwa walisema misaada inayotolewa inakwenda moja kwa moja kwa walengwa.

“Kwani ukijenga shule na zahanati si watatumia waathirika hao na hiyo ndiyo misaada yenyewe. Fedha zote zilizochangishwa na wahisani mbalimbali, wakiwamo wabunge kwa ajili ya kusaidia waathirika hao, zimetumika kwa ajili ya kuwasaidia ikiwemo kujengea shule na hospitali zilizobomoka kutokana na tetemeko hilo,” alisema Mavunde.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Wete(CUF) Mbarouk Salim Ali, alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuzuia na kupunguza athari yanapotokea maafa katika maeneo yaliyopitiwa na bonde la ufa na milima mikubwa.

Akijibu swali hilo, Mavunde alisema taarifa za kijiolojia zimeweka wazi uwezekano wa kutokea matetemeko 150 hadi 1,500 duniani ndani ya mwaka mmoja.

Kutokana na taarifa hizo, alisema tayari serikali imechukua hatua na kuweka mikakati ya kukabiliana na maafa hayo pindi yanapotokea.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi, iifanya tathmini ya kuainisha maeneo yenye viashiria vya uwezekano wa kukabiliwa na majanga katika nchi nzima.

“Serikali kwa kutambua uwezekano wa kutokea kwa majanga kama hayo, imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea,”alisema Mavunde.

Hata hivyo, alisema serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa iliyoainisha aina mbalimbali za maafa, ikiwamo tetemeko la ardhi na jukumu la kila mdau katika kushughulikia masuala ya afya.

Pia alisema serikali imeandaa mwongozo wa taifa wa kukabiliana na maafa unaoelekeza taasisi ongozi wajibu wao wakati wa kukabili maafa.

No comments:

Post a Comment