Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo
tarehe 17 Februari, 2017 amekutana na Makamu wa Rais wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati Bw.
Amadou Hott ambaye yupo hapa nchini kwa mazungumzo na wataalamu na
viongozi yenye lengo la kuboresha sekta ya nishati hususan uzalishaji wa
umeme.
Bw.
Amadou Hott amekuja nchini ikiwa ni utekelezaji wa mazungumzo
yaliyofanywa kati ya Mhe. Rais Magufuli na Rais wa AfDB Bw. Akinwumi
Adesina Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 31 Januari, 2017 ambapo
viongozi hao walikubaliana kuongeza ushirikiano kati ya AfDB na
Tanzania katika maendeleo huku mkazo ukielekezwa kupata majawabu ya
kuongeza uzalishaji wa umeme na wa gharama nafuu.
Bw.
Amadou Hott ameelezea kuguswa na dhamira ya Mhe. Rais Magufuli juu ya
kuongeza uzalishaji wa umeme na wenye gharama nafuu kwa ajili ya
kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda,
na ameahidi kuwa Benki hiyo itahakikisha dhamira hiyo inafanikiwa.
Kwa
Upande wake Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Amadou Hott kuwa
Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote
itakapohitajika ili kufanikisha dhamira hiyo.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa
Bharti Enterprises inayomiliki kampuni ya simu ya Airtel Duniani Bw.
Sunil Bharti Mittal ambapo viongozi hao wamezungumzia utendaji kazi wa
kampuni ya simu ya Airtel Tanzania ambayo Serikali ya Tanzania inamiliki
asilimia 40 ya hisa za kampuni hiyo.
Baada
ya mazungumzo hayo, Bw. Sunil Bharti Mittal ameelezea utayari wake wa
kuingiza kampuni ya Airtel Tanzania katika soko la hisa la Dar es Salaam
ili Watanzania wapate fursa ya kumiliki kampuni hiyo kwa kununua hisa.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapa nchini Mhe. Jean Pierre
Tshampanga Mutamba Ikulu Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment